Tamko la Wanafunzi wa Vyuo VikuuDodoma Kulaani Kuhusishwa KwaoKumshawishi Lowassa KuchukuaForm ya Uraisi

TAMKO LA UONGOZI WA SERIKALI ZA
WANAFUNZI WA VYUO VIKUU DODOMA KULAANI
KUHUSISHWA KWA WANAFUNZI WA VYUO VIKUU
VYA DODOMA NA KUMUOMBA MH.  LOWASA
KUGOMBEA URAIS.
Ndugu Waandishi wa habari, Tunapenda
kutanguliza shukrani za dhati kwenu kwa
kufika
katika eneo hili kutusikiliza.Mbele yenu ni viongozi
wa serikali za wanafunzi kutoka Vyuo vikuu
mbalimbali vilivyopo mkoani Dodoma.Ndugu
waandishi wa habari,si kawaida na wala mazoea
kwa marais na viongozi wa serikali za wanafunzi
kutoka vyuo tofauti kukutana kwa pamoja na
kuzungumza na nyie wanahabari kama
inavyotokea hii leo.
Ndugu wanahabari,siku ya Jumapili ya tarehe 22
mwezi huu wa 3,kundi la watu waliojitambulisha
kama ni wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma
walijikusanya nyumbani kwa mh; Lowasa na kutoa
matamko mbalimbali ikiwa pamoja na kuutangazia
uma wa watanzania kuwa sisi wanafunzi wa vyuo
vikuu vya Dodoma tunamuunga mkono na
tunahitaji Lowasa awe rais wetu sambamba
kumchangia pesa.
Ndugu wanahabari,Tunapenda kukanusha kuwa
wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma kwa ujumla
wetu hatukuhusika na jambo lile na kama viongozi
wa serikali za wanafunzi kutoka vyuo vikuu vya
mkoa huu wa Dodoma,Tunapinga na kulaani
kitendo cha watu wachache kwenda kutuingiza
sisi wanafunzi wa vyuo vikuu vya Dodoma katika
jambo ambalo halituhusu na wala si lililotuleta
hapa Dodoma.Sisi kama wasomi ambao jamii
inatutegemea kama kioo hatuwezi kuandamana na
kujikusanya kwenye nyumba ya kiongozi na
kumuomba agambee urais, wakati tunajua fika sisi
hatuhusiki na uteuzi wa wagombea ndani ya
taasisi yao.Kilichofanyika ni kuudanganya uma wa
watanzania na taasiasi yake kupitia kivuli cha
vijana wachache kutoka vyuo vya hapa
Dodoma,waliolipwa pesa ili waweze kuwa kava la
tukio lile.
Ndugu wanahabari,Mkoa wa Dodoma unavyuo
vikuu visivyopungua 8,Na jumla ya wanafunzi
wote tunaosoma katika vyuo vya Dodoma ni zaidi
ya wanafunzi  35,000.Chuo kikuu cha Dodoma
(UDOM) pekee yake kinawanafunzi wasiopungua
22,000.Idadi ya watu waliojikusanya nyumbani
kwa Mh: Lowasa siku ya tarehe 22-03-2015
haizidi watu 230 wakiwemo Wamachinga na
Wenyeviti wa Jumuiya za wazazi, kama vyombo
vya habari vilivyoripoti. Ukiwatoa Wamachinga na
Wenyeviti wa Jumuiya za wazazi waliotoka mikoa
mbalimbali,idadi ya wanafunzi waliokuwepo
kwenye tukio lile hawazidi 150.Idadi hii ni sawa na
asilimia 0.4 ya wanafunzi wote wanaosoma vyuo
vikuu vya Dodoma.Ndugu wanahabari,kwa akili ya
kawaida kabisa asilimia 0.4 ya wanafunzi wa vyuo
vikuu ndio waliokuwa pale.Tunashangazwa na
dhambi tusiyoitenda tunayobebeshwa wanafunzi
wa vyuo vikuu vya Dodoma ambao kwa sasa tupo
bize na msimu mpya ya masomo wenye
changamoto mbalimbali.
Ndugu wanahabari,sisi kama vijana wasomi na
watu tunaotegemewa na jamii zetu tutakusanyika
katika kujadili na kuchambua changamoto
mbalimbali zinazoikabili jamii yetu na sio
kukusanyika kwa ajili ya mwanasiasa ambaye sifa
zake na uhadilifu wake unatiliwa shaka katika
jamii.Tunaomba mlijulishe Taifa, kuwa wanafunzi
wa vyuo vikuu vya Dodoma hatujahusika na tukio
lile isipokuwa wanafunzi wachache walitumika
kwa kupewa pesa na wahusika wa tukio
lile.Tunataka Taifa lijue hatupo tayari kutumia
elimu zetu kulitia upofu taifa letu.Waambieni mama
zetu na baba zetu huku vijijini kwetu kuwa
tumekuja kutafuta elimu ili ituwezeshe
kuwakomboa wao na sio kutumika na Wanasiasa
kwa malengo yao.Tunatambua haki ya
mwanafunzi kuamua na kufanya shughuli za
kisiasa nje ya maeneo ya vyuo, lakini
hatukubaliani na wanafunzi wachache kuchafua na
kuwapaka matope maelfu ya wanafunzi wa vyuo
vikuu vya Dodoma ambao hawajahusika na tukio
lile.Hii sio haki na haikubaliki.
Vilevile tungependa kutumia fursa hii kuwaasa
wanafunzi wenzetu popote pale nchini, makundi
mbalimbali ya kijamii (wakulima, wafugaji, wavuvi,
wamachinga, wasanii, n.k), zikiwemo taasisi za
dini kwamba watu wachache kuzungumza kwa
niaba ya makundi juu ya mambo yanayogusa
maamuzi ya mtu binafsi.
Mwisho tunatoa wito kwa wanafunzi wenzetu wote
kujitambua na kutumie muda wetu kwa mambo ya
msingi na muhimu kwa ustawi wa Nchi yetu. Na
kuonesha jinsi wanafunzi wa Vyuo Vikuu vya
Dodoma walivyokasilishwa na jambo hili, Tamko
hili limesainiwa na wanafunzi 7821 toka vyuo mbali
mbali vya Dodoma.Majina ya sahihi za wanafunzi
zimeambatanishwa. Tusikubali kutumika na
wanasiasa wa aina hii..
Asanteni
Mungu ibariki Tanzania,Mungu vibariki vyuo vikuu
vya Dodoma.
Kwa niaba ya wawakilishi wa serikali za
Wanafunzi Chuo cha Mipango,Chuo cha Madini,
Chuo cha Hombolo,Chuo kikuu cha Dodoma
(UDOM) na CBE.

No comments:

Post a Comment