Siku tano baada ya Rais Jakaya Kikwete kusema kuwa tamko la Jukwaa la
Wakristo (TCF) kuwataka waumini wao kupigia kura ya ‘hapana’ Katiba
Inayopendekezwa lilikuwa la hasira, viongozi hao wamejitokeza tena na
kusisitiza kwamba msimamo wao huo utabaki kama ulivyo.
Katika tamko pamoja walilolitoa jana baada ya kukutana juzi mjini
Dodoma, viongozi hao wamemtahadharisha Rais Kikwete kuwa kuendelea
kupigia debe Katiba Inayopendekezwa na kuruhusu Mahakama ya Kadhi,
kunaweza kulitumbukiza Taifa katika machafuko na hali ikiwa hivyo
Serikali ndiyo itakayolaumiwa.
Tamko hilo limesainiwa na viongozi walewale waliosaini lile la awali la
Machi 12, mwaka huu ambao ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania
(CCT), Askofu Dk Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa
Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na
Mwenyekiti wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet.
Tamko lao hili hapa:
Sisi, Maaskofu kutoka TEC, CCT na CPCT tumekutana leo tarehe Machi 30,
2015 hapa Dodoma ili kuomba kwa pamoja juu ya mgawanyiko unaodhihirika
wa dini za Kikristo na Kiislamu kutokana na muswada wa Mahakama ya
Kadhi.
Maaskofu tuliokutana hapa hatuna hasira na wala hatuongozwi na hasira
wala mihemko katika kufikia maamuzi tunayofanya kama ambavyo wengine
wanavyotutafsiri.
Tunafikia maamuzi yetu baada ya maombi na sala na tunasukumwa na upendo
kwa wananchi ili kujenga taifa lenye umoja, amani, utulivu na maelewano.
Pia tumekuja kufuatilia kwa kina Muswada wa Marekebisho ya Sheria
Mbalimbali ya 2014 unaopendekeza, pamoja na mambo mengine, marekebisho
ya Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu la mwaka 1964.
Muswada huu unapendekeza kuanzishwa Mahakama ya Kadhi ambao
utawasilishwa Bungeni April 01, 2015 kwa hati ya dharura na hivyo
kuufanya umma wa Watanzania kutokujua maudhui yaliyomo katika muswada
huo wakati bado hoja zetu za msingi tulizopeleka kwenye Kamati ya Katiba
na Sheria ya Bunge na kwa Waziri Mkuu hazijajibiwa.
Tangu tulipokutana Machi 10, 2015 ambako tulitoa tamko letu kuhusiana na
Mahakama ya Kadhi na Katiba Inayopendekezwa, tumekuwa tukiendelea
kutafakari juu ya yale tuliyokuwa tumesema katika matamko yetu
mbalimbali na jinsi amani na utulivu wa nchi yetu vinavyoendelea
kumomonyoka siku zinavyokwenda.
Kwanza tumeshangazwa na tabia ya viongozi wa serikali ya kuitisha na
kuendesha mikutano wanayodai ni ya viongozi wa dini lakini isiyo rasmi.
Machi 03, 2015 Waziri Mkuu aliitisha mkutano kupitia Mchungaji mmoja
ambapo hakuna hata kiongozi mmoja wa taasisi au Kanisa aliyeshiriki.
Jambo la kushangaza ni kile kilichotokea Machi 28, 2015 ambapo Mhe. Rais
alishiriki kikao cha kikundi ambacho sio rasmi yaani Kamati ya Amani ya
Mkoa wa Dar es Salaam.
Tunasema kamati hiyo siyo rasmi kwa sababu haina baraka za viongozi wa
ngazi za juu wa kidini wa Mkoa huo na haina mwongozo wa kazi zake.
Mikutano ya jinsi hii kati ya serikali na wale ambao imewaona kuwa ndio
viongozi wa dini sio sahihi kwani viongozi wa dini wana taratibu zao za
kualikwa au kuwakilishwa katika mikutano na viongozi wa serikali au wa
dini au madhehebu mengine.
Tunawashauri wanaohutubia na wanaoshiriki mikutano hii wajue kwamba
washiriki hawana uwezo wa kuamua au kukubaliana na jambo lolote kwa
niaba ya viongozi wao wa juu na pia viongozi husika wa serikali
wasifurahi kwamba ujumbe wao umewafikia viongozi wa dini kwani hao
washiriki sio wawakilishi rasmi na hawana uwezo wa kutoa maamuzi au
kukubaliana juu ya jambo fulani la kitaifa.
Pili, tumekuwa tukifuatilia kwa karibu juu ya muswada wa Mahakama ya
Kadhi na tumebainisha dhahiri kwamba kile tulichokuwa tunasema kitatokea
kimeaanza kutokea bayana.
Yale yaliyotokea kwenye semina kuhusu Mahakama ya Kadhi kwa Waheshimiwa
Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Machi 29, 2015 ambao
ni wasomi, ni ishara ndogo sana ya kile kitakachotokea maeneo yote ya
nchi yetu. SERIKALI KWA NIA MOJA NA KWA SABABU TUSIZOZIJUA INAANZISHA
VITA VYA KIDINI KATI YA WATANZANIA WAKRISTO NA WAISLAMU.
Tunashangazwa kuona jinsi serikali inavyonuia jambo hili ovu
litakaloleta balaa kwa nchi yetu wakati huu wa kuelekea kura ya Maoni ya
Katiba Inayopendekezwa na baadaye Uchaguzi Mkuu wa 2015.
Kutokana na mambo hayo makuu mawili hapo juu, sisi Maaskofu wa Jukwaa la Wakristo Tanzania tunatamka kama ifuatavyo :
1.Matamshi ya Mhe. Rais akihutubia aliyowaita viongozi wa dini tarehe
Machi 28, 2015 kuwa Mahakama ya Kadhi ni ya Waislamu wenyewe na serikali
haitajihusisha wala kugharamia yanakinzana na kile kinachoendelea
bungeni na nchini.
Hapa tunajiuliza, endapo maneno ya Rais ni kweli, mbona Bunge
linaendelea kujadili kitu ambacho serikali haitajihusisha wala
kukigharimia ? Kwa mantiki hiyo, tunamtaka Mhe. Rais aagize muswada huu
uondolewe Bungeni na usijadiliwe tena kwa kuwa Utafiti wa Tume ya
kurekebisha sheria ulishaonyesha madhara ya uanzishwaji wa Mahakama ya
Kadhi.
Vinginevyo, kuendelea kujadiliwa kwa muswada huu maana yake ni kwamba serikali inajihusisha na itagharimia mahakama hiyo.
2.Serikali ijue kuwa endapo Wabunge wa dini za Kikristo na Kiislamu
watapigana na kisha baadaye wananchi nao wakafanya hivyo katika maeneo
yao, SERIKALI ITAKUWA NDIYO CHANZO CHA MAPIGANO HAYO.
Kama tulivyotamka hapo juu, kuhusiana na jambo hili tunamtaka Mhe. Rais
aiepushe nchi yetu na kuingizwa kwenye mapigano ya kidini ambayo
kuyadhibiti itakuwa vigumu sana (tafadhali rejea kinachoendelea huko
Nigeria).
Pia tunamwomba Mhe. Rais akumbuke na kutafakari kile kilichotokea na
kinachotokea nchi ya Afrika ya Kati kati ya kundi la Seleka (Waislam) na
kundi la Anti Balaka (Wakristo).
3.Tunaamini kuwa viongozi wa serikali wanafahamu viongozi rasmi wa dini
na madhehebu ya dini. Kwa mantiki hiyo tunawashauri viongozi wa serikali
waache kabisa kutumia vikundi visivyo rasmi kualika mikutano
wanayodhani kuwa itakubalika na waumini wa dini hizo. Mikutano yote ya
jinsi hiyo itakayoitishwa ni batili na maamuzi yake hatuyatambui na
hatutayatambua.
4.Bado Maaskofu tunasimamia Tamko letu la Machi 10, 2015 na tunawahimiza
Wakristo wajitokeze kwa wingi katika kujiandikisha katika Daftari la
Kudumu la wapiga Kura na zaidi wajitokeze kwenda kupiga kura ya HAPANA
wakati wa kura ya maoni kwani Katiba inayopendekezwa ilifikia hapo kwa
njia ya ubabe, ilikosa uadilifu na mbaya zaidi ni RUSHWA YA AHADI YA
MAHAKAMA YA KADHI ya iliyotolewa na Waziri Mkuu kwa Waislamu wakati wa
kupitisha Katiba Inayopendekezwa.
Tunafanya hivyo kwa dhamiri safi kwa sababu ya imani yetu na kwamba sisi
ni raia wa nchi hii na tuna haki ya kueleza mawazo yetu bila woga kama
Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 inavyotupa haki.
5.Mwisho tunawaomba Wakristo wote waendelee kufunga na kuomba kwa ajili ya utulivu na amani ya nchi yetu.
No comments:
Post a Comment